#EXCLUSIVE na Jokate : Afichua kuhusu baba wa mtoto, ndoa na malezi ya familia yake
Inapotajwa orodha ya vijana wanasiasa ambao nyota zao zilianza kung’ara katika Serikali ya Awamu ya Tano, Jokate Mwegelo ni miongoni mwa watakaokuwepo kwenye orodha hiyo.
Ni kati ya wakuu wa wilaya vijana ambao wameonyesha uwezo mkubwa kiutendaji na kuzidi kujenga imani kwa vijana kwamba wanapopata nafasi wanaweza kufanya makubwa.
Machoni mwa wengi mwanadada huyu alianza kuonekana katika mashindano ya urembo akitwaa mataji ya Miss Kurasini, Miss Temeke na hatimaye akaibuka mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka 2006.
Sanaa haikuishia hapo kwa Jokate kwani alionekana pia kwenye filamu na muziki baadaye akajitosa kwenye siasa na mwaka 2017 kuteuliwa kuwa kaimu katibu wa idara ya uhamasishaji na chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM.
Nafasi hiyo alidumu nayo kwa miezi na kuondolewa na kukaa benchi kwa miezi mitatu kisha jina lake likawa kwenye orodha mpya ya wakuu wa wilaya iliyotolewa na Rais John Magufuli Julai 2018 akiteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mwaka 2016.
Hatua zote alizopitia kwenye urembo, burudani na hata siasa alikuwa yeye kama yeye lakini mwishoni mwa mwaka 2022 akapata mtoto ambaye kwa kiasi fulani amebadili taswira na mwenendo wa maisha yake.
Mwananchi ilifunga safari hadi Korogwe ambako ndiko anakohudumu sasa kama mkuu wa wilaya na kufanya naye mahojiano maalum akieleza mambo kadha wa kadha kuhusu ujio wa mtoto wake, maisha yake kwa sasa na mtazamo wake kuhusu ndoa na familia.