NIONGOZE BWANA MUNGU-318.
OMBA UONGOZI WA MUNGU
Mara nyingi tunapoamka na kulala bila kuwa na hitilafu yoyote katika miili yetu; hujiona wenye nguvu na imara sana. Wakati mwingine hujisahau na kujikuta tukijisifu na kujitukuza kwa vipawa, karama, uchumi mzuri, baraka za watoto wazuri, wake/waume wazuri, cheo, na umaarufu.
Mambo ya aina hii humsababisha mtu kujiona ni mwenye kufanikiwa mno na pengine kupata kiburi. Kila mara unapoanza kuwa na kiburi hebu jiulize maswali yafuatayo:-
A. Ni kitu gani kinachonipa kiburi?
B. Kitanifikisha wapi hata nikiruhusu kuwa nacho?
C. Nani aliyewahi kuwa na kiburi na akaishia kufanikiwa?
D. Kuna haja ya kuwa na kiburi?
Nadhani mfalme Daudi alijiwekea tahadhari kubwa kwa kusema manano haya katika kitabu cha Zaburi 39:4 kuwa, "BWANA, unijulishe mwisho wangu, Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; Nijue jinsi nilivyo dhaifu."
Maneno haya yanaonesha namna ambavyo Daudi alimwogopa na kumtegemea Mungu. Katika maisha yetu kamwe tusijiinue wala kujisifu kwa lolote. Hii ni kutokana na kwamba maisha yetu yameshikiliwa na neema ya Mungu tu.
Wewe unaye dhani una haki ya kumdharau mwingine kumbuka kwamba huyo unayemdharau hakupenda kuwa hivyo. Lakini pia, wewe unayejiona una haki ya kuwatesa wengine, usijidanganye kabisa huwezi kuutesa uumbaji na mwenye nao akuangalie tu!
Maandiko katika kitabu cha 1 Petro 5:5 imeandikwa hivi, "Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema."
Unapotafakari neno hili hebu ungana nami kuimba wimbo namba 318. Wimbo unatukumbusha kuomba uongozi wa Mungu katika nyakati zote.
Ubarikiwe