Sherehe ya Watakatifu Wote: Wito Wa Utakatifu Wa Maisha!
Sherehe ya Watakatifu Wote: Wito Wa Utakatifu Wa Maisha!
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Novemba anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Wote, wito na mwaliko kwa watu wote kuchuchumilia ukamilifu wa maisha kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu, kwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu, daima wakijitahidi kumwilisha Matunda ya Roho Mtakatifu katika uhalisia wa maisha yao.
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha sherehe ya watakatifu wote. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema kwamba, Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha kutoka katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Wosia huu wa kitume umegawanyika katika sura kuu tano: Sura ya kwanza ni Wito wa utakatifu; Sura ya Pili ni Adui wa utakatifu; Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu, Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo na Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi!
Somo la kwanza (Ufu 7:2-4, 9-14) linatoka katika Kitabu cha Ufunuo. Linaleta kwetu maono ambayo Yohane mwenyewe aliyapata alipokuwa katika kisiwa cha Patmo. Kati ya yale aliyoyaona kuhusu ulimwengu ujao, aliona umati mkubwa wa watu wasiohesabika kutoka katika kila taifa, kabila na lugha. Wote wamesimama mbele ya kiti cha mwanakondoo wakiwa na mavazi meupe wakishika matawi mikononi mwao. Akaendelea kuona na kusikia kuwa watu hao ni wale waliotoka katika dhiki ile iliyo kuu na ni hao ambao wameosha mavazi yao katika damu ya huyo mwanakondoo. Tangu mwanzo Kanisa limeona maono hayo kuwa ni maono ya watakatifu huko mbinguni. Ni wa idadi isiyohesabika kwani ni wengi na kutoka kila sehemu. Mwanakondoo ndiyo alama ya Kristo mshinda, kama yule mwanakondoo wa Pasaka ya wayahudi, yeye ndiye aliyewakomboa hao umati kwa damu yake Msalabani. Nao wameupokea utakaso wake, wakawa tayari kuyaosha mavazi yao, yaani kutakaswa maisha yao yote kwa fumbo la Kristo la Pasaka. Ni somo linalotupa matumaini makubwa ya kuufikia utakatifu na ni somo linatoa hapo hapo mwaliko wa kuandamana na mwanakondoo, yaani Kristo katika maisha yetu yote.
Somo la pili (1Yn 3: 1-3) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa watu wote. Mtume huyu ambaye sehemu kubwa sana ya mafundisho yake ni upendo wa kimungu, leo anatufundisha kuwa ni pendo hilo alilotujalia Mungu linalotufanya sisi tuwe watoto wake. Kwa pendo lake Mungu tunafanyika watoto wa Mungu tukingali hapa duniani. Hadhi hii lakini huufikia ukamilifu wake huko mbinguni ambapo hatutakuwa tu watoto wake bali tutamwona jinsi alivyo na kufanana naye milele yote. Wanaomwona Mungu jinsi alivyo na wanaofanana naye ni watakatifu wake. Kumbe Yohane naye anatukumbusha kuwa tunayo tayari ndani yetu amana ya utakatifu kwa pendo ambalo Mungu anatupenda sisi. Na kama ulivyo mwaliko wa kudumu wa mtume Yohane, tukae katika pendo la Mungu ili tuufike ukamilifu wa kuwa waana wake, yaani kumuona Yeye kama alivyo na kufanana naye milele yote.
Injili (Mt 5:1-12A) somo la Injili ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo na ni maarufu kama Injili ya Heri nane. Heri hizi Yesu anazitoa kama katiba ya ufuasi au mwongozo wa tunu za maisha ambazo kila mfuasi wake anapaswa kuwa nazo ili astahilishwe kuishiriki ile heri ya umilele, yaani utakatifu. Mwinjili Mathayo anapozitaja na kuzifundisha heri hizi nane, anaweka msisitizo wa heri kama fadhila za maisha ya kiroho. Hii ni tofauti kidogo na mwinjili Luka anayezifundisha kama fadhila za maisha ya kijamii. Utofauti huu sio upinzani. Kwa mwinjili Mathayo, kuziishi heri ni kuyaishi maisha yaliyo na kipimo cha juu kidogo kuliko yale maisha ya kawaida ya kijamii. Ni utofauti huo unaosisitizwa kama fadhila za kiroho. Mwisho, ni muhimu kutambua kuwa Yesu anapozitaja na kuzifundisha heri hizi, anajitambulisha Yeye mwenyewe kuwa ndiye mfano wa kuziishi heri hizo. Ndiye hasa aliye masikini wa roho, ndiye aliyejua huzuni, ndiye aliye mpole, ndiye aliye na njaa na kiu ya haki, ndiye mwenye huruma, ndiye msafi wa moyo, ndiye mpatanishi na ndiye mwenye kuudhiwa kwa ajili ya haki. Kwa jinsi hii anaonesha kuwa maisha ya heri sio nadharia. Yanawezekana. Na ni Yeye aliyetoa mfano wa kuyaishi. Hivyo anatualika nasi tuyaishi ili tupate kustahilishwa kuishiriki ile heri ya milele.